Friday, 12 September 2014

Mara Milele: Zaidi ya watu 300,000 wanatarajiwa kuhudhuria maadhimisho ya siku ya Mara (Mara Day Celebrations)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Zaidi ya watu 300,000 wanatarajiwa kuhudhuria Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara (Mara Day) yatakayofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara,  Jimbo la Narok, Jamhuri ya  Kenya.

Maadhimisho ya siku ya Mara huadhimishwa kila mwaka kwa pamoja kati ya Tanzania na Kenya ambazo ni Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hufanyika kwa pamoja ili kusherehekea mazingira ya Mto Mara na faida zake kwenye maisha yao.

Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yamepangwa kufanyika tarehe 15th Septemba, 2014 na yatahudhuriwa na watu mashuhuri kutoka Tanzania na Kenya, wawakilishi kutoka serikali za majimbo ya Narok na Bomet, Mkoa wa Mara, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria(LVBC), Mashule, Sekta Binafsi na wawakilshi wa  asasi za Kijamii.

Tarehe “15th Septemba  ilikubaliwa na Baraza la Mawaziri la kumi(10) la Kisekta ya Bonde la Ziwa Victoria  Tarehe 4 Mei,2012 Kigali – Rwanda kuwa siku ya Mara yaani  ‘Mara Day’.

Maelekezo ya Baraza yanaongeza chachu kwenye utekelezaji wa sera ya usimamizi endelevu wa Mto Mara na Mazingira yake katika Bonde la Ziwa Victoria” na juhudi za Nchi za Tanzania na Kenya na serikali ya majimbo ya Narok,Bomet na Mkoa wa Mara hazina Budi kupongezwa kwa maandalizi ya siku hii yatakayopelekea kufanikisha maadhimisho haya.

Serikali za Tanzania na Kenya na Wadau wa maendeleo kama vile Shirika la Maendeleo la Kimarekani (USAID), World Wide for Nature (WWN), Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program (NELSAP) na Sekta binafsi zimekuwa msaada mkubwa katika kuendeleza Mazingira ya Mto Mara.  

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya wameahidi kushirikiana katika usimamizi endelevu wa Bonde la Mto Mara kama mazingira ya kiasili katika bonde la Ziwa Victoria linalochangia katika maendeleo endelevu ya kijamii, utunzaji mazingira na uhai wa uchumi wa nchi hizi. 

LVBC wanachukulia juhudi za ushirikiano wa Nchi hizi Wanachama kama hatua muhimu za kusimamia na kuendeleza rasilimali za jamii zilizozunguka maeneo haya ili kuweza kuchangia katika agenda za mtangamano wa Afrika Mashariki.   

Sekta binafsi na Asasi za Kijamii zinazozunguka jamii hizi sio tu kushiriki katika siku ya Mara bali kushiriki kikamilifu katika usimamizi endelevu wa mto Mara kwa kuwa maisha ya mamilioni ya watu na viumbe mbalimbali vya Hifadhi maarufu duniani ya Serengeti na mbuga ya Maasai Mara yanategemea ustawi wa Mazingira haya.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu ni “Mara Milele” na maadhimisho haya yanafanyika kipindi hiki muafaka ambacho uhamaji mkubwa wa Nyumbu na Wanyama wengine, ambapo inakadiriwa jumla ya Nyumbu milioni mbili(2) wanahama kutoka mbuga ya Serengeti- Tanzania kwenda mbuga ya Maasai – Mara Kenya kwa kipindi cha Julai mpaka Octoba kila Mwaka. Uhamaji huu ni kati ya Maajabu saba mapya ya Dunia.

Maadhimisho ya tatu(3) ya siku ya Mto Mara  yatatanguliwa na mkutano na vyombo vya habari, kupanda mti, michezo mbalimbali na shughuli nyingine ili kufanikisha maadhimisho haya. Matukio haya yatafanyika kama sehemu ya kuadhimisha Mto Mara kama rasilimali ya kikanda kwa maendeleo endelevu ya Bonde la Ziwa Victoria na kuongeza uelewa kwa wadau kwenye changamoto na umuhimu wa bonde la Mto Mara. 

Maazimisho haya ya Mto Mara yanalenga kujenga uelewa wa ekologia Mto huu kama rasilimali ya pamoja ya kikanda baina ya Nchi hizi mbili kwa kuwezesha wadau wa Mto mara umuhimu wa utunzaji bonde la mto Mara na viumbe vilivyomo kwa maendeleo ya Jamii zinazozunguka maeneo haya na Taifa kwa Ujumla.
    
“Maadhimisho ya Mto Mara yanapelekea mwonekano wa  mali asili zilizoko katika ukanada wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na umuhimu uliopo kwenye maliasili hii kwa maisha ya viumbe na uchumi wa Nchi hizi mbili.


IMETOLEWA NA WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI