Monday, 23 May 2016

Mkutano wa Sita wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanza Leo Jijini Arusha, Tanzania.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Simu ya maandishi: ‘MEAC’
Simu Na. 022-2126827, 2126830, 2126823
Fax: 022 – 2126651/2120488
Barua Pepe: ps@meac.go.tz
Tovuti: www.meac.go.tz

NSSF Waterfront Ghorofa ya 5
35 Barabara ya Edward Sokoine
S.L.P 9280,
11467 DAR ES SALAAM,
Tanzania.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Sita wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanza Leo Jijini Arusha, Tanzania.

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeanza Mkutano wake leo Mei 23, 2016 Jijini Arusha, Tanzania. Mkutano huu wa Sita, Kikao cha Nne wa Bunge la Tatu unatarajiwa kufanyika kwa siku 12 kuanzia leo Jumatatu Mei, 23 hadi Ijumaa Juni 3, 2016.

Bunge hili katika Vikao vyake linatarajiwa kuongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mhe. Daniel Kidega. Moja kati ya ajenda kuu katika Bunge hili ni kusomwa kwa Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Mei 26, 2016. Baada ya bajeti kusomwa watajadili na kupitisha Bajeti hiyo ikiwa ni moja ya sehemu ya majukumu yaliyopo kwenye Mamlaka yao.

Hotuba ya Bajeti ni shughuli muhimu katika utekelezaji wa Kalenda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mwaka wa fedha 2015/2016 EALA ilijadili na kupitisha makadirio ya Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jumla ya Dola za Kimarekani 110,660,098.

Bajeti ya mwaka 2015/2016 ilitoa kipaumbele katika utekelezaji wa hatua mbili muhimu za Mtangamano; Himaya ya Umoja wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja ambayo ililenga kuipandisha hadhi Pasi ya kusafiria ya Afrika Mashariki  kuwa ya Kimataifa, kuboresha mazingira ya biashara ndani ya Jumuiya, na kuboresha mfumo wa malipo.

Katika hatua nyingine EALA katika Mkutano wake wa wiki mbili linatarajiwa kuhutubiwa na Wake wa Marais Waasisi wa Jumuiya ambao ni Mama Maria Nyerere (Mke wa Baba wa Taifa na Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mw. Julius Kambarage Nyerere), Mama Maria Obote (Mke wa Rais wa zamani wa Uganda Hayati Milton Obote) na Mama Ngina Kenyatta (Mke wa Rais wa zamani wa Kenya Hayati Jomo Kenyatta). Katika tukio hili litakalo fanyika Mei 30, 2016 pia itakuwa ni fursa pekee kwa Wabunge wa EALA na watendaji wengine mbalimbali kubadilishana uzoefu na Wake wa Marais Wastaafu, ikizingatiwa kuwa Jumuiya ya sasa imechukua misingi muhimu ya kiutendaji kutoka kwa Jumuiya ya awali.

Katika Bunge hili la Sita Muswada wa Sheria wa watu wenye ulemavu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia unatarajiwa kujadiliwa.

Aidha, Bunge linatarajia kupokea na Kujadili ripoti mbalimbali kutoka kwa kamati zake. Ripoti hizo ni pamoja na;
·         Ripoti kutoka kamati ya Mawasiliano Biashara na uwekezaji na,
·         Ripoti kutoka kamati ya malengo ya pamoja,

Vilevile Bunge litasimamia vikao vya majadiliano ya kamati zake juu ya misuada na Masuala mbalimbali ya Jumuiya katika kipindi chote cha wiki mbili za Mkutano wake.Thursday, 5 May 2016

Kikao cha Kumi na Nne cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda, 29 Aprili – 1 Mei, 2016

Kikao cha Kumi na Nne cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda, 29 Aprili – 1 Mei, 2016


Kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilifanyika kuanzia tarehe 29 Aprili hadi Aprili, 2016, Mjini Gisenyi, Rwanda, ambapo wataalam wa sekta mbalimbali waliazimia kuharakisha maeneo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Kikao hicho cha 14 cha ushirikiano kimefanyika kufuatia maagizo ya Marais wa Tanzania na Rwanda wakati wa ziara ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli nchini Rwanda mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

Wakati wa ziara hiyo, wakuu hao walikubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuinua shughuli za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha wataalamu kiongozi wa ujumbe wa Tanzania Balozi Ramadhan M. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania aliwakumbusha wajumbe wa pande zote mbili kuendesha mazungumzo na mjadala kwa kuzingatia maagizo ya viongozi hao na vilevile kuchangamkia fursa za ushirikiano wa shughuli za kiuchumi za wananchi wa pande zote mbili baada ya mindombinu ya kikanda kuimarika.

Kwa upande wake, Balozi Jeanine Kambanda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda na mwenyeji wa kikao hicho, alihimiza wajumbe kujiwekea malengo yanayotekelezeka na tarehe za ukomo kwenye maeneo yote watakayokubaliana ili kusukuma utekelezaji na kupata matokeo ya haraka.

Pamoja na mambo mengine, pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu kama vile miundombinu ya ushoroba wa kati (central corridor), kuharakisha ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa (standard gauge), kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya mashirika ya ndege ya Rwandair na ATCL, kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo na ufugaji, utalii, elimu, mawasiliano n.k.

Mkutano huo pia umekubaliana kuanzisha Kamati ya Pamoja ya Utekelezaji (Joint Implementation Committee) kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu maeneo yote ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika Kikao hicho cha 14. Kamati hiyo itakayoongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizo mbili, itakutana kila robo mwaka.

Aidha, Serikali ya Rwanda imeonesha utayari wake wa kuleta nchini Maafisa na Watumishi wa Serikali kwa lengo la kupata uzoefu na mafunzo katika vyuo vya kitaalamu nchini kama vile Chuo cha Diplomasia  (CFR), Chuo cha Taifa cha Utalii na Wanyamapori  (Mweka) na Chuo cha Usafirishaji (NIT).

Kwa upande wa Tanzania, Serikali imedhamiria kuwakutanisha wataalamu wa mitaala ya elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na Rwanda kwenye upande wa kuandaa mitaala ya elimu ya tehama kwenye shule za awali, msingi na sekondari.

Mkutano ujao wa kumi na tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda utafanyika mwaka 2018, nchini Tanzania.

WAKATI HUO HUO, Kikao cha pamoja cha Makatibu Wakuu kati ya Tanzania na Zambia kwa ajili ya kujadili utatuzi wa changamoto za mpaka wa Nakonde Tunduma kilifanyika Lusaka Zambia 25 hadi 27 Aprili, 2016.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano  huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius Likwelile na kwa upande wa Zambia uliongozwa na Bw. Bright Nundwe, Katibu Mkuu wa Jimbo la Muchinga.

Miongoni mwa changamoto zilizojadiliwa na ufumbuzi wake wakati wa mkutano huo ni pamoja na:- Msongamano wa magari ambapo kwa  upande wa Zambia huduma kwa magari ya mizigo zinafanyika hadi saa nne usiku na kwa magari ya abiria huduma inatolewa kwa masaa 24. Ili kupunguza msongamano, Tanzania imeiomba Zambia kutoa huduma kwa magari ya aina zote kama Tanzania inavyotoa huduma ya masaa 24; na Kuimarisha usalama mpakani ili kukabiliana na biashara haramu za kubadilisha fedha, biashara za magendo na biashara haramu za binadamu.

Mwisho, pande zote mbili zilikubaliana suala hilo lishughulikiwe kwa kufanya ukaguzi na ulinzi wa pamoja na kubadilishana taarifa za kiusalama.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,

 05 Mei, 2016