JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO
WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
|
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara ya Mhe. Salva Kiir, Rais wa Jamhuri ya Sudan
Kusini Tarehe 15 Aprili 2016
Mhe. Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan
Kusini atafanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania tarehe 15 Aprili
2016. Rais Kiir anakuja nchini kusaini Mkataba wa kuwezesha Jamhuri ya Sudan
Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo
tangazo la kukubaliwa kuwa Mwanachama wa EAC lilitangazwa na Mwenyekiti wa
Jumuiya hiyo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha
mwezi Machi 2016.
Rais Kiir atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere saa 3:00 asubuhi na baadaye ataelekea Ikulu na
kupokelewa na Mwenyeji wake, Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli. Baada ya
hapo, Viongozi hao watashiriki hafla ya uwekaji saini ya Mkataba huo
iliyopangwa kuanza saa 5:00 asubuhi na kisha watapata fursa ya kutoa hotuba na
kusaini Communique.
Rais wa Sudan Kusini atashiriki hafla ya chakula
cha mchana kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake kabla ya kuondoka
nchini baada ya hafla hiyo.
Sudan Kusini ni nchi ya sita kujiunga na Jumuiya ya
Afrika Mashariki, ambapo inaongeza fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza
kuzifaidisha Nchi Wanachama ikiwemo Tanzania, endapo mipango madhubuti itawekwa
kuzichangamkia. Fursa hizo ni pamoja na za kibiashara kwa kuwa bidhaa nyingi
zinazotumika Sudan Kusini zinaagizwa kutoka Nje ya nchi. Hivyo, jamii ya
wafanyabiashara wa Tanzania wanahimizwa kuchangamkia fursa zinazopatikana
nchini humo na ndani ya Jumuiya kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 14 Aprili, 2016
No comments:
Post a Comment