Monday, 23 May 2016

Mkutano wa Sita wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanza Leo Jijini Arusha, Tanzania.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Simu ya maandishi: ‘MEAC’
Simu Na. 022-2126827, 2126830, 2126823
Fax: 022 – 2126651/2120488
Barua Pepe: ps@meac.go.tz
Tovuti: www.meac.go.tz

NSSF Waterfront Ghorofa ya 5
35 Barabara ya Edward Sokoine
S.L.P 9280,
11467 DAR ES SALAAM,
Tanzania.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Sita wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuanza Leo Jijini Arusha, Tanzania.

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeanza Mkutano wake leo Mei 23, 2016 Jijini Arusha, Tanzania. Mkutano huu wa Sita, Kikao cha Nne wa Bunge la Tatu unatarajiwa kufanyika kwa siku 12 kuanzia leo Jumatatu Mei, 23 hadi Ijumaa Juni 3, 2016.

Bunge hili katika Vikao vyake linatarajiwa kuongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mhe. Daniel Kidega. Moja kati ya ajenda kuu katika Bunge hili ni kusomwa kwa Hotuba ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Mei 26, 2016. Baada ya bajeti kusomwa watajadili na kupitisha Bajeti hiyo ikiwa ni moja ya sehemu ya majukumu yaliyopo kwenye Mamlaka yao.

Hotuba ya Bajeti ni shughuli muhimu katika utekelezaji wa Kalenda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mwaka wa fedha 2015/2016 EALA ilijadili na kupitisha makadirio ya Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jumla ya Dola za Kimarekani 110,660,098.

Bajeti ya mwaka 2015/2016 ilitoa kipaumbele katika utekelezaji wa hatua mbili muhimu za Mtangamano; Himaya ya Umoja wa Forodha na Itifaki ya Soko la Pamoja ambayo ililenga kuipandisha hadhi Pasi ya kusafiria ya Afrika Mashariki  kuwa ya Kimataifa, kuboresha mazingira ya biashara ndani ya Jumuiya, na kuboresha mfumo wa malipo.

Katika hatua nyingine EALA katika Mkutano wake wa wiki mbili linatarajiwa kuhutubiwa na Wake wa Marais Waasisi wa Jumuiya ambao ni Mama Maria Nyerere (Mke wa Baba wa Taifa na Rais wa awamu ya kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mw. Julius Kambarage Nyerere), Mama Maria Obote (Mke wa Rais wa zamani wa Uganda Hayati Milton Obote) na Mama Ngina Kenyatta (Mke wa Rais wa zamani wa Kenya Hayati Jomo Kenyatta). Katika tukio hili litakalo fanyika Mei 30, 2016 pia itakuwa ni fursa pekee kwa Wabunge wa EALA na watendaji wengine mbalimbali kubadilishana uzoefu na Wake wa Marais Wastaafu, ikizingatiwa kuwa Jumuiya ya sasa imechukua misingi muhimu ya kiutendaji kutoka kwa Jumuiya ya awali.

Katika Bunge hili la Sita Muswada wa Sheria wa watu wenye ulemavu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia unatarajiwa kujadiliwa.

Aidha, Bunge linatarajia kupokea na Kujadili ripoti mbalimbali kutoka kwa kamati zake. Ripoti hizo ni pamoja na;
·         Ripoti kutoka kamati ya Mawasiliano Biashara na uwekezaji na,
·         Ripoti kutoka kamati ya malengo ya pamoja,

Vilevile Bunge litasimamia vikao vya majadiliano ya kamati zake juu ya misuada na Masuala mbalimbali ya Jumuiya katika kipindi chote cha wiki mbili za Mkutano wake.



No comments:

Post a Comment