Wednesday, 13 August 2014

Maonesho ya Juakali/NguvuKazi ni zaidi ya kuuza bidhaa

Kamati ya maandalizi ya maonesho ya 15 ya Juakali/Nguvukazi yakutana Jijini Kigali-Rwanda, mkutano huu ulioanza tarehe 30 Julai-August 1, 2014 katika ukumbi wa sports view hotel Kigali-Rwanda, lengo kuu la mkutano huu ikiwa ni kuandaa maonesho ya 15 ya Juakali/Nguvukazi yanayotarajiwa kuanza tarehe 1-7 Disemba,2014 katika Viwanja vya Gikondo-Rwanda.
Akifungua mkutano huu mwenyekiti Bi. Gladys Kinyuah kutoka Kenya alisema lengo kuu la maonesho haya si wajasiliamali kuuza bidhaa zao tu bali ni uwanja wa kubadilishana technologia, uzoefu na masoko, “wakati umefika sasa tuwaambie wajasiliamali wetu tunapofanya maonesho haya si kwenda kuuza bidhaa tu bali ni kutafuta masoko na kubadilishana ujuzi na technologia mpya kutoka kwa wenzetu”. Akifafanua Bi Gladys alitoa mfano wa Nchi zilizoshamiri kiuchumi kutokana na mchango wa sekta isiyo rasimi, nchi kama Marekani,Japan na Malasia wajasiliamali wana mchango mkubwa kwa kukuza uchumi wa Nchi hizo, mfano Japan sekta isiyo rasmi inachangia 80% ya uchumi wa nchi hiyo na hii ni kutokana na Nchi hiyo kuithamini na kuipa kipao mbele sekta hii muhimu.
Kamati ya maandalizi imekubaliana kwa mwaka huu maonesho haya yawe zaidi katika kumsaidia mjasiliamali kujua jinsi ya kutafuta masoko, kunadi bidhaa zake na kuhakikisha wanazingatia viwango ambavyo vitawawezesha kuuza bidhaa zao ndani ya Nchi za Afrika Mashariki na kwenye masoko ya Kimataifa.
 Ili kuwapa uwezo wajasiliamali wa Juakali/Nguvukazi kamati ya Maandalizi imekubaliana kutakuwa na kongamano la siku mbili litakalofanyika tarehe 1 na 3 Disemba, 2014 kwenye viwanja vya maonesho Rwanda ili kuweza kutoa elimu ya masoko na taratibu nyingine kwa wajasiliamali na kushirikishana shuhuda za wajasiliamali waliofanikiwa kwa kupitia maonesho ya Juakali, elimu hiyo itatolewa na wataalamu wa masoko kwa njia ya kuwasilisha na majadiliano.
Takwimu za ajira zinaonesha 80% ya ajira katika Nchi za Afrika Mashariki zianatoka katika sekta isiyo rasimi (MSEs), wakati umefika sasa sekta hii muhimu kwa Nchi za Afrika Mashariki kuaangaliwa kwa jicho la tatu.
Maonesho ya JuaKali/NguvuKazi ni maonesho yanayohusisha wajasiliamali wadogo kutoka Nchi za Afrika Mashariki, maonesho haya hufanyika kila mwisho wa mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kwa kila Nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa maonesho hayo. Maonesho haya yalianza tangu mwaka 1999 ikiwa ni mawazo ya wakuu wa Nchi waazilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Tanzania, Kenya na Uganda na baadae Rwanda na Burundi kujiunga, Mwaka huu maonesho haya yanatimiza miaka 15.
Wajasiliamali wanahimizwa kuhakikisha wanaboresha biashara zao hasa katika ufungaji wa biashara zao (Packaging) na kuonesha ubunifu wa hali ya juu ili kuweza kuipa thamani bidhaa na kuwezesha bidhaa hizi kuuzwa hata kwenye masoko ya Kimataifa, kwani kuna bidhaa nyingi nzuri zinazozalishwa na wajasiliamali wadogo ila huwa zinapoteza sifa kwa masoko ya nje sababu ya kukosa baadhi ya vigezo, hivyo ni vyema tukahakikisha tunapambana na changamoto hizo kwa kufuata taratibu zote na kuwa wabunifu ili tuweze kukuza uchumi wetu na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana.

No comments:

Post a Comment