Kuelekea uchaguzi Mkuu Nchini unaotarajiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba, 2015 Jumuiya ya Afrika Mashariki imeleta timu ya waangalizi yenye jumla ya watu 55 inayohusisha wataalamu na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo wastaafu na wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka nchi wanachama. Timu hii iliwasili Jijini Dar es Salaam 18 Oktoba, 2015.
Katibu Mkuu Bibi Joyce Mapunjo akizungumza kwenye Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana katika Hoteli ya New Afrika Jijini Dar es Salaam ambao pia ulihudhuriwa na waangalizi kutoka EAC na SADC amewahimiza waangalizi wa uchaguzi kuzingatia sheria na taratibu za Nchi katika shughuli zao.
Akizungumza katika mkutano huo alisisitiza kuwa Tanzania ni Nchi ya Kidemokrasia na inautaratibu mzuri wa kuachiana madaraka ambapo uchaguzi hufanyika kila baada ya miaka mitano na kubadilsha uongozi wa juu kila baada ya miaka kumi kwa mujibu wa katiba.
Kiongozi wa timu ya Uchunguzi kutoka EAC ambaye pia ni Makamu wa Rais wa zamani wa Kenya Mhe. Dkt. A. A Mood Awori akizungumza katika Mkutano huo aliipongeza Tanzania kwa kudumisha Demokrasia na Utawala wa kisheria na kuongeza kuwa katika uchaguzi huu Tanzania iendeleze utamaduni wa kudumisha Demokrasia, Utawala Bora na uwajibikaji ili iendelee kuwa na amani na utulivu.
Timu ya waangalizi ya EAC ambayo itafanya kazi katika vipindi vitatu vinavyotajwa kuwa, Kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi itaangalia mambo yafuatayo;
· Ushirikishwaji wa vyombo vya habari katika kuripoti masuala mbalimbali ya uchaguzi
· Muda wa kutosha wa kampeni
· Uhuru wa kuendesha shughuli za kisiasa pasipo fujo au vitisho
· Utolewaji wa elimu ya uraia na upigaji kura
· Upigaji kura kwa siri, na
· Ubora wa vifaa vya uchaguzi
Aidha timu hiyo ya waangalizi itafanya kazi yake Tanzania bara na Visiwani wakati wote wa uwepo wake katika kipindi chote cha uchaguzi.
No comments:
Post a Comment