Friday, 18 March 2016

BUNGE LA EALA KUWAENZI WAKE WA WAASISI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limepitisha kwa sauti moja hoja ya kuwaenzi wake wa Marais Waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyopita (1967-77), wake hao ni Mama Maria Nyerere (Tanzania), Mama Ngina Kenyata(Kenya) na Mama Mirium Obote (Uganda).
 Hoja hii iliwasilishwa Bungeni na Mhe. Mumbi Ng’aru kutoka Kenya, hoja hii wakati ikiwaslishwa ilivuta hisia za wabunge wengi, akiongea wakati anawasilisha hoja hiyo aliomba Bunge kuunga mkono hoja hiyo na kuwaalika katika kikao cha Bunge kinachotarajiwa kufanyika Mei, 2016 Jijini Arusha.

Akiongea wakati anawailisha hoja hiyo alisema wakati umefika sasa Bunge kutambua mchango wa wakina mama hawa wanaobeba historia kubwa ya Jumuiya, kwani wakati Marais hawa wanahangaika na harakati za kuunganisha nchi za Afrika Mashariki wao walikuwa bega kwa bega na Marais hawa kuwasaidia hasa katika kuwashauri vizuri na kuaangalia familia, huu ni ukweli usioweza kufumbiwa macho, kwani akina mama hawa wameendelea kutoa mchango wao kwa Mataifa yetu na Jumuiya yetu ya sasa kwa kutoa viongozi ambao wanaitumikia Nchi zetu na Jumuiya yetu kwa namna moja au nyingine.

“Nilibahatika kuzungumza na akina mama hawa kwa nyakati tofauti, na kwa kweli akina mama hawa ni zaidi ya maktaba ya masuala ya Afrika Mashariki, ni hadhina ambayo tuna kila sababu ya kujivunia” alisema Mhe. Mumbi. Wabunge kwa sauti moja walikubaliana akina mama hawa kualikwa katika Kikao cha Bunge kitakachofanyika Arusha na kuhutubia Bunge hilo.

Wabunge wengine waliochangia hoja hii kutoka Tanzania ni Mhe. Shyrose Bhanji, Mhe. Makongoro Nyerere na Mhe. Nderakindo Kessy.

Katika hatua nyingine Bunge limepitisha ripoti ya Kamati ya Masuala ya Sheria, ripoti hiyo iliyohusu uoanishaji na uhuishaji wa Sheria za ndani ya Nchi wanachama na zile za Jumuiya, akichangia wakati wa majadiliano kuhusu ripoti hii Mhe. Abdullah Mwinyi alisema utekelezaji wa hatua mbalimbali za Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa umoja wa forodha na Soko la Pamoja utategemea zaidi kuhuishwa kwa sheria hizi kwani sheria nyingi za Nchi wanachama zinakinzana na zile za Jumuiya hivyo kufanya utekelezaji kuwa mgumu na wanaoathirika zaidi ni wananchi ambao ndio watumiaji wa sheria hizo.


Bunge hili lilianza vikao vyake tarehe 7 Machi,2016 na kukamilisha Vikao vyake Jana tarehe 17 Machi, 2016, pamoja na mambo mengine Musuada wa kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu (EAC Counter Trafficking in Persons Bill,2016), ulisomwa kwa mara ya kwanza.

No comments:

Post a Comment