Tanzania Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mara nyingine
Katika Hoteli ya Ngurugoto Jijini Arusha Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya
Mwenyekiti Mhe. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania imeombwa na wakuu wa Nchi hizo kuendelea kushikilia kiti hicho kwa Mwaka mwingine.
Mhe. Rais John Pombe Magufuli akisisitiza jambo |
Mkutano huo ambao ulikuwa wa kipekee kutokana na jinsi Mwenyekiti alivyoeendesha Mkutano, umejadili na kupitisha maamuzi mbalimbali, kati ya maamuzi hayo ni pamoja na kuchagua Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mkutano huu kutokana na matakwa ya Mkataba wa Jumuiya unaoelekeza kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya atakaa na cheo hicho kwa kipindi cha Miaka mitano(5).
Hivyo mkutano huu umemteua Bw. Liberat Mfumukeko kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, madaraka hayo ataanza rasmi kuyatumikia tarehe 26 Aprili,2016 tarehe ambayo Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Richard Sezibera atakuwa amemaliza kipindi chake.
Mkutano huu vilevile uliridhia maombi ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Jamhuri ya Sudan Kusini, kuridhia kwa maombi haya kunafanya Jumuiya sasa kuwa na Nchi wanachama sita(6). Wakiongea kwa nyakati tofauti Wakuu hawa wa Nchi waliipongeza Nchi ya Sudan ya Kusini na kuwakaribisha katika Jumuiya. “Kila Nchi ina matatizo yake cha muhimu ni kuvumiliana na kuheshimiana ili tuweze kufikia lengo letu la kuwaletea Wanaafrika Mashariki maeendeleo, tunawakaribisha sana wenzetu kutoka Jamhuri ya Sudan, kujiunga kwa Sudan ya Kusini kunafanya Jumuiya kuwa na soko la watu zaidi ya Millioni 150” alisema Mwenyekiti.
Vilevile Mkutano huu umemteua Rais Msataafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Benjamini Wiliam Mkapa kuwa mwezeshaji wa mazungumzo ya kuleta amani Nchi ya Burundi.
Katika Mkutano huu Mwanafunzi Mtanzania Simon S. Mollel kutoka shule ya Sekondari ya Mzumbe alitunikiwa cheti na pesa taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani 1500 kwa kuwa mshindi wa kwanza wa shindano la Insha la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushindi wa pili ulichukuliwa na mwanafunzi kutoka Kenya, wa tatu kutoka Rwanda, wanne kutoka Uganda na wa tano kutoka Burundi wote hawa walitunikiwa vyeti na pesa taslimu.
Wakuu wa Nchi katika mkutano huu walizindua Pasi mpya ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Pasi hii itakuwa ya kisasa kabisa na itaweza kutumika duniani kote, hivyo Wanaafrika Mashariki hawatalazimika kuwa na pasi nyingine, pasi hii inatarajiwa kuanza kutumika rasmi tarehe 1 Januari,2017.
Akiongea katika hotuba ya kufunga mkutano huu wa 17 wa Wakuu wa Nchi, Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi Mhe. John P. Magufuli, aliwasihi watendaji wa Secretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuzingatia matumizi mazuri ya pesa, aliwakumbusha kuwa hizi ni pesa za walipa kodi wa Afrika Mashariki hivyo ni vyema wakazingatia matumizi mazuri ya pesa, alitoa mfano wa matumizi ya ukumbi wa Hoteli ya Ngurudoto ambao ni ghali badala yake Mkutano huu ungeweza kufanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa ‘AICC’ ambao ni bei rahisi na ni Mkubwa.
Akimalizia alisema “ tunatakiwa kuhakikisha kila mwanaafrika mashariki ananufaika na fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki, tusiwe Jumuiya ya kuwanyonya wananchi, yeyote ambaye ataenda kinyume na kuzingatia utaratibu huo sitasita kumripoti kwa Wakuu wa Nchi wenzangu ili atumbuliwe”.
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakuu wa Nchi walimpongeza sana Mhe. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyeti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jinsi alivyoeendesha Mkutano huu kwa ustadi.
No comments:
Post a Comment