JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI,
KIKANDA NA KIMATAIFA
Simu ya maandishi: ‘MEAC’
Simu Na. 022-2126827, 2126830, 2126823
Fax: 022 –
2126651/2120488
Barua Pepe: ps@meac.go.tz
Tovuti: www.meac.go.tz
|
NSSF Waterfront Ghorofa ya 5
35 Barabara ya Edward Sokoine
S.L.P 9280,
11467 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
MKUTANO WA NNE WA BUNGE
LA TATU LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUANZA JIJINI ARUSHA
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki linatarajia kuanza mkutano wake Jijini Arusha, Tanzania. Mkutano huu wanne wa Bunge la tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (BJAM) utafanyika kwa siku kumi na mbili (12) kuanzia leo Jumatatu Januari 24, 2016 hadi Ijumaa Februari 5, 2016.
BJAM ambalo litaongozwa na spika wake Mhe. Daniel F. Kidega, katika vikao vyake litajadili taarifa kutoka kamati mbalimbali zenye mapendekezo kuhusu hatua mbalimbali za mtangamano kutoka kwa wadau sambamba na kujadili taarifa za kamati zifuatazo;
· Taarifa ya Kamati ya Malengo ya Pamoja inayozungumzia kuhusu maombi ya vibali vya kazi na uraia, kufuatia mapendekezo ya Shirikisho la Wafanyakazi la Afrika Mashariki na Chama cha Waajiri Afrika Mashariki.
· Kupokea na kujadili taarifa kutoka Kamati ya Sheria na Kinga kuhusu mapendekezo ya maboresho na marekebisho ya kanuni mbalimbali za BJAM.
Katika hatua nyingine wakati wa Mkutano huu wa Bunge kutakuwa na zoezi la kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Dkt. Suzan Kolimba ili aweze kushiriki katika Vikao vya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, BJAM linatarajia kupokea na kujadili Musuada wa kupunguza majanga ya mwaka 2013 (Disaster Risk Reduction Bill 2013).
Vilevile, suala la mgogoro wa kisiasa wa Nchini Burundi unatarajiwa kuwa sehemu ya mjadala katika Mkutano huu wa nne wa Bunge hilo. Kamati ya Bunge ya Masuala ya Kikanda na Usuluhishi wa migogoro itamalizia na kuwasilisha taarifa iliyoipokea kutoka Chama cha Wanasheria cha Umoja wa Afrika inayohusu hali ya kisiasa Nchini Burundi.
Katika BJAM Tanzania inawakilishwa na Wabunge Tisa; Mhe. Charles Makongoro Nyerere ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, Mhe. Issa Twaha Taslima ambaye ni Katibu, wengine ni Mhe. Abdullah Ally Hassan Mwinyi, Mhe. Shy-Rose Sadrudin Bhanji, Mhe. Adam Omar Kimbisa, Mhe. Angela Charles Kizigha, Mhe. Bernard Musomi Murunya, Mhe.Perpetua Kessy Nderakindo na Mhe. Maryam Ussi Yahya
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki linafanya Mikutano yake kwa utaratibu wa Mzunguko miongoni mwa Nchi wanachama kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 55 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha BJAM linakutana kwa Mwaka mara moja katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha, Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
Dar es Salaam, Januari 23, 2016
No comments:
Post a Comment