MWINYI KUWA MWENYEKITI WA JOPO LA UANGALIZI WA UCHAGUZI UGANDA.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk. Richard Sezibera amemwomba Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Al Hassan Mwinyi kuwa Mwenyekiti wa Jopo la waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Nchini Uganda.
Dr. Sezibera alisema hayo alipomtembelea Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dk. Balozi Aziz Mlima ofisini kwake kwa lengo la kumuelezea nia ya mazungumzo yake na Rais Mwinyi ikiwa ni pamoja na masuala mengine ya Jumuiya kuhusu Mkutano Mkuu wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya.
Aidha Dk. Sezibera katika mkutano wake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amesema Rais Mwinyi amekubali ombi hilo na kumuomba Katibu Mkuu wa Wizara kusaidia kutafuta msaidizi wa Rais Mwinyi atakaye kuwa msemaji mzuri ukizingatia kipindi cha uchaguzi vyombo vya Habari huwa na mambo mengi yakufuatilia katika uchaguzi utakaofanyika mapema mwezi ujao.
Pamoja na maelezo yake kuhusu masuala ya Uchaguzi Nchini Uganda Dk. Sezibera alizungumzia kuhusu kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Mawaziri na Mkutano wa Kilele wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajia kufanyika Jijini Arusha tarehe 29 mwezi wa pili na kumueleza kuwa utakuwa mzito sana na wa aina yake kufuatia mkutano huo kuunganishwa na mkutano mwingine muhimu wa masuala ya bajeti ya Jumuiya.
Pamoja na Mambo mengine pia agenda za Mkutano Mkuu huo zitaangalia masuala ya maombi ya Sudan ya Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, masuala ya Jumuiya kufikia shirikisho la kisiasa, kuzindua hati ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye hadhi ya kimataifa pamoja na mapitio ya muundo wa Sekretariati ya Jumuiya.
Mkutano huu uliotakiwa ufanyike mwishoni mwa mwaka jana kwa mujibu wa kalenda ya kazi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliahirishwa kufuatia muulingiliano wa ratiba za uchaguzi uliokuwa ukiendelea miongoni mwa nchi wanachama ikiwemo Tanzania, na badala yake utafanyika Februari 29, 2016.
No comments:
Post a Comment