Wednesday, 27 January 2016

MHE. Dkt. SUZAN KOLIMBA ALA KIAPO BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI



MHE. Dkt. SUSAN KOLIMBA ALA KIAPO BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI.
Mhe. Naibu Waziri Dkt Susan Kolimba akila kiapo 26/01/2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa amekula kiapo leo katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, kiapo hiki kinamuwezesha kushiriki vikao vya Bunge kama Mbunge anayeingia kwa nafasi yake (Ex-Officio Member) hii ni kwa mujibu wa sheria namba 5 ya Sheria za Bunge hilo, kiapo hicho kilitolewa mbele ya Spika wa Bunge hilo Mhe. Daniel F. Kidega.


Baada ya kiapo Mhe. Dkt Susan alichukuwa nafasi yake kama mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri katika Kikao hicho. Akiongea baada ya kuchukuwa nafasi yake Mhe. Dkt. Kolimba amelihakikishia Bunge hilo kwamba Tanzania itahakikisha inashiriki kikamilifu katika hatua zote za Mtangamano ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuanzisha Jumuiya hii kwa faida ya WanaAfrika Mashariki. 



‘Kama ilivyo kauli mbiu ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya “Hapa kazi tu”, sisi kama wenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tunawahakikishia wanaafrika Mashariki tutaeenda kwa kasi ya Hapa kazi tu ili kuhakikisha Mtangamano huu unakuwa na faida kwa Wanaafrika Mashariki wote’ alisema Mhe. Dkt. Kolimba.


Aidha, katika hatua nyingine katika kikao hicho kutokana na ratiba, bunge lilikuwa linajadili musuada wa sheria ya kupunguza majanga ya mwaka 2013 (Disaster Risk Reduction Bill 2013). 

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki Dkt. Susan A. Kolimba kwa niaba ya Baraza la Mawaziri aliomba musuada huo kutojadiliwa na kusogezwa mbele ili kulipa nafasi Baraza la Mawaziri kuweza kuboresha zaidi muswada huo, baada ya majadiliano wabunge waliridhia maombi ya Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Musuada huo utajadiliwa tena Machi, 2016 baada ya Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kufanya maboresho.

Bunge la Afrika Mashariki ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichoanzishwa chini ya Ibara ya 9 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki( The Treaty for the Establishment of East African Community). Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki linafanya Mikutano yake kwa utaratibu wa Mzunguko miongoni mwa Nchi wanachama kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 55 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha BJAM linakutana kwa Mwaka mara moja katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Arusha, Tanzania.

Mhe. Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba (mwenye Biblia mkononi) akila kiapo mbele ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki linaloendelea Jijini Arusha.
Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Daniel F. Kidega (aliyesimama) akiendesha vikao vya Bumge hilo. 
Mhe. Naibu Waziri Susan Kolimba (katikati) akisindikizwa na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Shy- Rose Sadrudin Bhanji (kushoto) na Mhe. Angela Charles Kizigha (kulia) wakati akienda kula kiapo mbele ya Bunge hilo.











No comments:

Post a Comment