Thursday, 2 October 2014

VIKWAZO NANE VYA KIBIASHARA VYAPATIWA UFUMBUZI
Jumla ya vikwazo visivyo vya kiushuru (NTBs) nane vilivyoripotiwa vimepatiwa ufumbuzi katika Mkutano wa 15 wa kikanda uliofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 25 - 27 Septemba, 2014.

Miongoni mwa vikwazo hivyo nane vilivotajwa kupatiwa ufumbuzi, vitatu kutoka Tanzania, kimoja kilihusu Nchi zote Wanachama na vinne Nchi nyingine wanachama.

Kwa upande wake Tanzania iliwasilisha taarifa ya kupunguzwa kwa idadi ya vituo vya mizani katika lango la kati ambavyo kwa sasa vimebaki sita kati ya 15 vya awali.

Hatua hii imechukuliwa sambamba na kuondolewa kwa vituo vya ukaguzi vya Polisi.

Katika mkutano huo Tanzania ilitoa taarifa ya kuongezwa kwa magari matano ya polisi kwa lengo la kuimarisha shughuli za doria katika lango la kati.

Aidha, katika mkutano huo vikwazo vingine vipya nane vya kibiashara viliripotiwa, kati ya hivyo vikwazo viwili viliripotiwa na Kenya dhidi ya Uganda, na Uganda dhidi ya Kenya iliripoti vikwazo vitano,na kikwazo kimoja kiliripotiwa na Tanzania dhidi ya Kenya.

Vikwazo vilivyoonekana kuleta utata Mkutano uliadhimia vilipelekwe kwenye Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afrika Mashariki la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji.

Miongoni mwa vikwazo vilivyotajwa kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri la Kisekta la Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji ni pamoja na kupima katika mizani magari matupu ya mizigo, Usajili wa bidhaa kutoka Mamlaka ya Dawa na Chakula, Mahitaji ya nembo au jina kutoka Mamlaka ya Dawa na Chakula na mahitaji ya chanjo ya homa ya manjano. 

Ilipendekezwa kuwa vikwazo vinavyolalamikiwa kutoka Mamlaka ya Dawa na Chakula vipelekwe Bodi ya Viwango ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata maoni ya kitaalamu yatakayosaidia kupatikana kwa ufumbuzi.

Kwa Upande wake Serikali ya Tanzania imedhamiria kupunguza idadi ya vituo vya mizani kutoka vituo sita vya sasa mpaka vituo vitatu ifikapo June 2015.

Na Teodos Komba

No comments:

Post a Comment