JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO
WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Kikao
cha Mwaka cha Menejimenti ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha UNICEF
jijini Dar es Salaam (25 – 29 Aprili 2016)
Waziri
wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga amelihakikishia Shirika La Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Watoto (The United Nations Children's Emergency Fund-UNICEF) kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na shirika hilo katika harakati zake za kuboresha ustawi, kutetea
na kulinda haki za watoto duniani.
Aliyasema
hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha mwaka cha Menejimenti ya
Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika cha Shirika hilo kilichoanza tarehe 25
Aprili na kinahitimishwa leo kwenye Hoteli ya Ramada.
Dkt.
Mahiga alisema kuwa UNICEF ni shirika kubwa linalojulikana duniani kwa mchango
wake katika ustawi wa nchi zinazoendelea, hususan katika kuhakikisha kuwa
watoto wanapata haki zao za kimsingi.
Waziri
Mahiga aliendelea kueleza kuwa katika kuhakikisha kuwa watoto wanapatiwa haki
zao ipasavyo, hakuna budi UNICEF ikashirikiana na Serikali husika kukabiliana
na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma harakati hizo. Alizitaja
changamoto kubwa kwa ustawi wa watoto ni
pamoja na sera, mifumo ya kisheria, ufinyu wa bajeti na urasimu katika taasisi
za Serikali. “Tunakabiliwa na changamoto nyingi katika harakati za kuimarisha
ustawi, kutetea na kulinda haki za watoto ambazo ili ziweze kutatuliwa kwa
wepesi lazima Serikali, UNICEF na wadau wengine tufanye kazi kwa pamoja”.
Waziri
wa Mambo ya Nje aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa kuna masuala mengi
yanayosababisha matatizo kwa watoto duniani ambayo yanatakiwa yatafutiwe
ufumbuzi kwa pamoja. Masuala hayo ni pamoja na usafirishaji haramu wa watoto,
biashara haramu ya dawa za kulevya, unyanyasaji dhidi ya wanawake, machafuko ya
kisiasa, kushindwa kuwawezesha wanawake na kuwahudumia watoto.
Alisema hayo na
masuala mengine yanasababisha changamoto kubwa kwa watoto. Aidha,
Dkt. Mahiga alizungumzia changamoto zinazowakabili watoto wa Tanzania ambazo ni
pamoja na mauaji ya watoto, hususan wenye ualbino, kuongezeka kwa watoto wa
mitaani, kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watoto ambako kunasababisha ukosefu
wa ajira, ukatili dhidi ya watoto na ukandamizaji wa haki nyingine za watoto.
Alishauri
UNICEF iwe na mikakati mahsusi ya kushughulikia changamoto zinazoikabili nchi
husika kwa kushirikiana na taasisi za nchi hiyo. Kwa upande wa Tanzania,
alisema kuwa inakabiliwa na changamoto ya mauaji ya watu wenye ualbino na
kuongezeka kwa mahitaji katika sekta ya elimu ili kuboresha ubora wa elimu,
kufuatia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwa sababu ya Serikali ya awamu ya
tano kutangaza elimu ya awali hadi ya sekondari bure.
Dkt.
Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa jambo kubwa linalomsumbua ni
kuhakikisha kuwa watoto katika kipindi cha ujauzito hadi miaka mitano wanaishi
bila kupoteza maisha kutokana na magonjwa na ukosefu wa lishe bora pamoja na
kuwalinda hususan katika maeneo ya machafuko.
Ziara ya Waziri wa Nchi wa
Viwanda na Biashara wa Singapore, Mhe Dkt. Koh Poh Kun nchini Tanzania tarehe 27 Aprili 2016.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi wa Viwanda na
Biashara wa Singapore Mhe Dkt. Koh Poh Kun amefanya ziara ya kikazi nchini tarehe 27 Aprili 2016. Pamoja na mambo mengine, Dkt. Koh amefanya
mazungumzo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa (Mb) mjini Dodoma. Katika mazungumzo yao, Dkt. Koh amemhakikishia Mhe.
Waziri Mkuu kwamba makampuni ya Singapore yataendelea kufanya uwekezaji katika
sekta mbalimbali nchini.
Hadi hivi sasa Makampuni ya Singapore
yaliyokwishawekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi
cha Dola za Kimarekani Bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza
zaidi dola za kimarekani Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata
gesi (LNG plant) kitakachojengwa kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na
Marekani.
Aidha, kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za
Kimarekani Milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa
makampuni ya gesi. Dkt. Koh pia alimfahamisha Mhe. Waziri Mkuu kwamba kampuni ya
Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi
(Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka
mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati
(light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo
37,000. Jiwe la Msingi la Mradi huo
litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji Mhe
Charles Mwijage (Mb).
Mbali na ushirikiano katika sekta ya Biashara na
Uwekezaji, Dkt. Koh amemfahamisha Mhe Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia
Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na
uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta. Alisema
Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya
kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa
bandari za Tanzania. Vilevile, Singapore imeahidi kuandaa mafunzo mahususi kwa
ajili ya Makatibu Wakuu wa Tanzania. Mafunzo hayo ya wiki moja yatatumika kubadilishana
uzoefu na makatibu wakuu wa Singapore pamoja na Mawaziri. Dkt. Koh alisema
Serikali ya Singapore inatoa kipaumbele cha juu katika kuwajengea ujuzi
watumishi wa umma kwasababu msingi wa mafanikio ya Taifa lao ni kuwa na rasilimali watu
walio na weledi,ujuzi,uzoefu
na uadilifu.
Kwa upande wake, Mhe Waziri Mkuu aliishukuru Serikali
ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada
ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano
za kukuza uchumi, Mhe Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore
kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuanzisha viwanda, hoteli, kilimo na nishati. Aidha, alimuahidi Dkt. Koh
kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia
na kulinda uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Bilateral Investment Protection
and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili (Avoidance
of Double Taxation Agreement) ili kuvutia uwekezaji zaidi kati ya mataifa hayo
mawili.
Kuhusu fursa za mafunzo, Mhe Waziri Mkuu ameiomba
Serikali ya Singapore itoe fursa zaidi katika mafunzo ya wataalam wa sekta za
gesi na uchukuzi.
Awali, Dkt. Koh alifanya mazungumzo na: Mwenyeji wake
Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb), Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof Makame Mbarawa (Mb), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) na Naibu Waziri wa Mambo
ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan
Kolimba (Mb).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam, 28 Aprili, 2016