Wednesday, 14 October 2015

WANACHAMA WAPYA WAWILI WAAPISHWA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.WANACHAMA WAPYA WAWILI WAAPISHWA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (BJAM) katika Mkutano wake wa pili (2), kipindi cha Nne (4) cha Bunge la tatu linaloendelea Jijini Nairobi; tarehe 7 Oktoba , 2015 lilisimamia kiapo cha utii wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wanachama wapya wawili (2) waliojiunga na Bunge hilo.

Bunge lilimwapisha Waziri wa Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki kutoka Jamhuri ya Burundi Mhe. Leontine Nzeyimana ambaye ameteuliwa tena kuiongoza Wizara hiyo.

Mhe. Dkt. Francois Xavier Kalinda, ambaye ni Mbunge mpya toka Nchini Rwanda pia aliapishwa katika Mkutano huo, kiapo kiliongozwa na Katibu wa BJAM Bw. Kenneth Madete mbele ya Spika wa Bunge hilo Mhe. Daniel F. Kidega.Wote wawili waliapa kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) ya Kanuni za Bunge la BJAM inayosema; “Hakuna Mbunge anaweza kukaa au kushiriki katika vikao vya Bunge mpaka hapo kiapo cha kudhihirisha utii kwa Mkataba kitakapo chukuliwa" (No Member can sit or participate in the proceedings of the House until the Oath or Affirmation of Allegiance to the Treaty is taken”)

Kabla ya kuchaguliwa na Bunge la Rwanda na kuapishwa kuwa Mbunge wa BJAM Mhe. Dkt. Kalinda, alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Mhe. Dkt Kalinda ameapishwa kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Celestine Kabahizi ambaye alijiuzulu Juni, 2015.

Aidha, Mhe. Leontine Nzeyimana, ameteuliwa kwa mara nyingine kuwa Waziri wa Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia uchaguzi uliofanyika Mwezi Julai Nchini Burundi. Mhe. Nzeyimana ameiongoza Wizara katika nafasi hiyo tangu mwaka 2012. Mhe. Nzeyimana ana Shahada ya Uzamili katika Mahusiano ya Kimataifa, ambapo kabla alisoma Shahada ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, Tanzania aliyohitimu mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment