ELIMU KWA UMMA NI MSINGI KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI- EALA
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki(BJAM) ambalo linaeendelea na vikao vyake Jijini Arusha, terehe 28 Januari, 2016 waliendelea na mjadala kuhusu ripoti iliyowasilishwa kuhusu kibali cha ukaazi/kufanya kazi (work / residence permit) katiki Nchi wanachama za Afrika Mashariki.
Katika mjadala huo kwa sauti ya pamoja Wabunge walisisitiza suala la elimu kwa umma kutiliwa mkazo kwa Nchi zote wanachama, wakichangia wabunge hao walisema suala la elimu kwa umma ni suala la Msingi sana kwani katika Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha 7 kinasema Jumuiya hii itakuwa ni Jumuiya ya watu na inayozingatia masoko “ The Community shall be people centered and Market driven” kwa kuzingatia hilo ni muhimu sana kwa wananchi kuelimishwa ili kuweza kuwa sehemu ya Jumuiya hii na kuweza kunufaika na matunda ya Jumuiya hii hasa ya Soko la pamoja.
Wakiongea katika mjadala huo wabunge walisema wakati mwingine wanachi wanajikuta katika matatizo hasa wanapotoka Nchi moja kwenda Nchi nyingine ya Afrika Mashariki kwa sababu hawajui taratibu na makubaliano yaliyofikiwa katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika Jumuiya.
Katika kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja kuna Mipaka, Soko la pamoja haimanishi kwamba kila kitu kitakuwa huru, kuna maeneo ambayo Nchi wanachama walikubaliana kushirikiana na wakati huohuo sheria na taratibu za Nchi mwanachama husika zinapaswa kuzingatiwa. Hivyo wananchi wanatakiwa kuelimishwa mipaka na makubaliano malimbali yaliyofikiwa katika Itifaki mbalimbali katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akichangia katika mjadala huo Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa upande wa Tanzania Mhe. Shyrose Bhanji, alisisitiza Nchi wanachama kuchangamkia fursa za Soko la Pamoja la Afrika Mashariki
“ Nashangaa ni Watanzania wangapi mfano wamechangamkia fursa ya kwenda kufundisha Lugha ya Kiswahili kwenye Nchi hizi za Afrika Mashariki? Ni wakati sasa umefika jitihada za kuhakikisha elimu kwa umma hasa kwa fursa zinazopatikana katika Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki inawafikia wananchi wote ili wananchi wengi waweze kupata fursa ya kufanya kazi katika Nchi Wanachama” alisisitiza Mhe. Shyrose.
Katika mjadala huo wabunge walitilia mkazo suala la kuhuisha sheria mbalimbali za ndani ya Nchi wanachama ili masuala mbalimbali yaliyokubaliwa katika Itifaki ya Soko la Pamoja yaweze kutekelezeka, hasa kuhakikisha ada za vibali vya ukaazi/kufanya kazi zinahuishwa ili wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waweze kufanyakazi au kuishi katika Nchi wanachama.
Wabunge hao wamehimiza Nchi wanachama kuhakikisha wanalipa kipao mbele swala la elimu kwa umma ili wananchi waweze kujua masuala mbalimbali katika Jumuiya, vilevile wametoa wito kwa wananchi wa Afrika Mashariki kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika Jumuiya hasa katika Soko la Pamoja wakati huohuo wakizingatia sheria na taratibu za Nchi husika kama ilivyo makubaliano katika Itifaki mbalimbali katika maeneo ya Ushirikiano.