Tuesday 19 January 2016

Tanzania: Tupo tayari kushiriki katika Mazungumzo ya Burundi


Tanzania: Tupo tayari kushiriki katika Mazungumzo ya Burundi.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Maiga akizumgumza na waandishi wa habari mwishoni wa wiki alisema Tanzania ipo tayari kushiriki katika mazungumzo ya kuiletea amani Burundi kadri itakavyo amliwa na Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika siku za karibuni.

Katika Mkutano huo na waandishi wa habari ambao pia alishiriki Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Mhe. Alain Aime Nyamitwe, Waziri Mhe. Balozi Dkt Maiga ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki alisema “nimempokea Waziri wa Burundi leo, sababu ya ujio wake ni kutoa ishara na uthibitisho kuwa Burundi iko tayari kutushirikisha katika kutafuta suluhu na amani tukiwa kama wenyekiti, ni jambo la kufurahisha pia kuona mazungumzo ya amani yanaendelea baina ya Warundi wenyewe, na kwa kuhusisha Mataifa mengine katika kuleta amani”. 

Aidha kwa upande wake Waziri wa mambo Mambo ya Nje wa Nchini Burundi Mhe.Alain Aime Nyamitwe katika Mkutano huo alisema Burundi ikotayari kuendelea na mazungumzo ya kuleta amani nchini humo kufuatia changamoto za kiusalama zinazo ikabili Nchi hiyo baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Julai 21, 2015.

“Hali ya Burundi ni salama, tunakabiliwa na changamoto chache za kiusalama katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Bujumbura lakini ukienda maeneo ya vijijini hali ni shwari kabisa na wananchi wanaendelea na kazi zao za kila siku kama kawaida na Serikali inajitahidi kufanya kila linalowezeakana kuhakikisha changamo hizi za kiusalama zinatatuliwa mapema iwezekanavyo” alisema Mhe. Nyamitwe. 

Aliongeza kusema Mazungumzo ya ndani ya Nchi na Msuluhishi yanaendelea pia kwa kuhushikisha makundi mbalimbali ya kijamii zikiwemo asasi za kiraia, viongozi wa dini na wananchi wote kwa ujumla.


Mhe. Nyamitwe aliwasili Jijini Dar es Salaam Ijumaa tarehe 15/01/2016 kumtembelea Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Maiga ambapo baada ya mazungumzo kwa pamoja waliongea na vyombo vya habari katika Mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi mdogo wa Mikutano wa Wizara. Kwa wakati huu Tanzania ni Mwenyeki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment