Kituo cha Holili chazinduliwa rasmi
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaoshughulilikia masuala yanayohusika na Vituo vya kutoa huduma kwa pamoja Mipakani wamezindua rasmi kituo cha Holili/Taveta katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Kituo hicho kilizinduliwa rasmi tarehe 27 Februari, 2016
|
Mhe. Waziri akikata utepe wa kuashiria kufunguliwa rasmi kwa
Jengo la OSBP la Holili.
Dhana ya Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani ni dhana ya kisasa inayohusu Nchi zinazopakana, kutoa huduma, uwezeshaji na udhibiti kama forodha, uhamiaji, usalama na afya kwa kushirikiana. Hivyo, abiria au msafirishaji bidhaa halazimiki kusimama na kukaguliwa au kukamilisha taratibu za udhibiti sehemu mbili tofauti wakati wa kutoka kwenye nchi moja na wakati wa kuingia nchi nyingine. Hatua hii inawezesha Idara, Taasisi na Wakala kutoka Tanzania na Nchi jirani zinazotoa huduma na udhibiti mpakani kufanya kazi kwa pamoja na hivyo kupunguza muda wa kukaa mpakani na kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha.
|
Kituo hichi kimejengwa kwa gharama zinazokadiliwa kuwa kiasi cha dola za Kimarekani 12 millioni ambao ni msaada kutoka kwa wahisani wa TradeMark East Africa (TMEA).
Kituo hiki kimefunguliwa rasmi kwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Kazi na Masuala ya Afrika Mashariki kutoka Kenya Bi. Phillis Kandie.
Akiongea katika ufunguzi huo Mhe. Balozi Dkt. Mahiga alisema, “inafurahisha kuona maafisa wa pande mbili wakifanya kazi kwa ushirikiano, hii hainoeshi ushirikiaono tu bali inadhihirisha umoja na udhihirisho wa kauli mbiu ya Jumuiya ya ‘Watu wamoja, hatima moja – one people one destiny’. Hivyo nawasihi watu wetu wa Kilimanjaro na Taveta kutumia fursa hii kikamlifu”.
Mhe. Waziri alisema Tanzania inathamini mchango wa Kituo hiki kwa kukuza biashara kati ya Tanzania na Kenya na kudhihirisha hilo Tanzania tayari imeridhia muswada wa kuongoza vituo hivi “OSBP Bill”.
Vituo hivi vitasaidia kupunguza muda hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara kwa wafanyabiashara, wakulima na wasafirishaji kutoka Nchi moja mwanachama kwenda Nchi nyingine.
Akiongeza alisema barabara ya Arusha-Holili/Taveta-Voi inayotarajiwa kuzinduliwa tarehe 3 Machi,2016 itaongeza biashara ya mipakani na kuchochea ujirani mwema kati ya Tanzania na Kenya.
Mhe. Alisema kinachofuata ni kuwajengea uwezo watendaji wa kuendesha vituo hivi ili waweze kutoa huduma kwa ufaanisi.
Akiongea katika ufunguzi huo Mhe. Kandie alisema pamoja na kuwawezesha wakulima na wafanyabiashara kutoka Kaskazini mwa Tanzania kwenda soko la Kenya, Kituo cha Holili/Taveta kitasaidia kuongeza mahusiano na umoja. “Nimefuraishwa na hatua ya ujenzi wa Barabara ya Taveta-Mwatate-Voi, ambayo imefikia 75%, na inatarajiwa mwisho wa mwaka huu kazi hii itakamilika na hivyo watu wa Taveta na Kaskazini mwa Tanzania watasafiri kwenda Mombasa na sehemu nyingine za Kenya bila matatizo”
Mhe. Kandie alisistiza kwamba vikwazo visivyo vya kiforodha ni tatizo na alisema serikali ya Kenya kwa kushirikiana na Nchi nyingine Wanachama wanajitahidi kutafuta njia mbalimbali za kuondoa vikwazo hivyo ili kufanya Jumuiya hii iwe ya kiushindani na kuvutia zaidi.
Akiongea katika ufunguzi huo Katibu Mkuu wa Jumuiya Dkt. Sezibera alisema Holili/Taveta ni kituo cha kwanza kuzinduliwa kati ya vituo (8) vilivyojengwa katika mipaka ya Nchi wanachama na vimekamilika vinasubiria kufunguliwa rasmi, alisema “ Jumuiya ya Afrika Mashariki iligundua kuwa uchumi wa Nchi hizi wanachama unategemeana hivyo njia nzuri ya kufanyakazi pamoja ni kupunguza gharama za kufanya biashara”.
Mr. Theo Lyimo, Mkurugenzi wa Vituo hivi kwa upande wa TMEA akiongea kwenye hafla hii aliwashukuru wahisani ambao wamesaidia mradi huu, wahisani hao ni - DFID, Canada, USAID and the World Bank.
“ Holili/Taveta ni kati ya vituo 15 Afrika Mashariki na Sudan ya Kusini vilivyojengwa kupitia ufadhili wa mradi wa TMEA, tumewekeza kiasi cha dolla za Kimarekani 117 million kinachofurahisha ni kwamba kati ya dolla 1 tuliyowekeza inatarajiwa kuleta dolla 30,” alisema Bw. Lyimo.
Hafla hii ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya na hafla hii ilifanyikia kwa upande wa Tanzania - Holili.