Saturday, 20 February 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara imepata taarifa zisizo na ukweli zinazoenezwa na kusambazwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa Wizara na Serikali kwa ujumla, kuwa Wizara iliyokuwa ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendesha zoezi la kukusanya wasifu(CV) za Wafanyakazi wake kwa lengo la kuwafukuza kazi. 

Wizara imesikitishwa na inalaani vikali uvumi wa taarifa hizi na inakanusha kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Zoezi la kukusanya CV za watumishi ni zoezi la kawaida kwa waajiri na hufanyika 

Mara kwa mara kwa lengo la kuhuisha sifa na uzoefu wa watumishi wanazopata wakiwa kazini ambapo hatimaye huwekwa kwenye majalada yao binafsi, mwajiri anapaswa kuhakikisha jalada la kila mtumishi lina taarifa zinazoeenda na wakati, hivyo zoezi hili lilifanyika kwa lengo la kuhuisha taarifa za watumishi wa Wizara kama ilivyoelekezwa na mwajiri na si vinginevyo.

Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuwa CV si miongoni mwa nyaraka zinazohitajika katika kumfukuza kazi mtumishi bali mtumishi anafukuzwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi ambapo taratibu maalumu za kinidhamu hufuatwa. Katika kipindi husika Wizara haina mtumishi anayetuhumiwa kwa kosa la kinidhamu linaloweza kupelekea kufukuzwa kazi, hivyo taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Aidha, Wizara inakemea vikali watu wenye tabia ya kutoa taarifa zisizo na ukweli na zenye kupotosha umma. Vilevile Wizara inapenda kuwaasa wananchi kuheshimu sheria na taratibu za Nchi sambamba na kutoeneza taarifa zinazotokana na vyanzo visivyokuwa rasmi au zisizothibishwa na mamlaka husika, kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na taratibu za Nchi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
19 Februari, 2016


No comments:

Post a Comment