Wednesday, 10 February 2016

MHE. NAIBU WAZIRI DKT. SUSAN KOLIMBA AKUTANA NA WABUNGE WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI (EALA) ARUSHA

Mhe. Naibu Waziri (wa tatu kulia) akiongea na Wabunge wa Afrika Mashariki kwa upande wa Tanzania kabla ya kuingia kwenye kikao cha Bunge, kulia kwake ni Mhe. Nderakindo Kessy, Mhe. Makongoro Nyerere, Mhe. Maryam Yahya na Mhe. Shyrose Bhanji na kulia kushoto kwake ni Mhe. Angela Kizigha akifuatiwa na Mhe. Bernard Murunya anayeandika ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango.
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Mtangamano na Utatuzi wa Migogoro Mhe. Abdullah A. Mwinyi akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo kusuhu changamoto za utekelezaji wa Soko la Pamoja, kulia kwake ni Mhe. Spika wa Bunge la EALA Mhe. Daniel Kidega aliekaa kiti cha peke yake na wengine ni waandishi wa Bunge .
Mhe. Dkt Susan Kolimba, Naibu Waziri Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa akimpongeza Naibu Waziri Mkuu wa tatu na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Uganda Mhe. Kirunda Kivejinja baada ya kuapishwa hapo jana kuwa Mjumbe maalum wa Bunge la Afrika Mashariki, katikati ni Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Burundi Mhe. Leontine Nzeyimana


TANZANIA YAPONGEZWA UONDOAJI WA VIKWAZO VISIVYO VYA KIFORODHA

Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki linaendelea na vikao vyake Jijini Arusha, Vikao hivyo vilianza tarehe tarehe 25 Januari, 2016 na Bunge hilo linatarajia kukamilisha shughuli zake tarehe 4 Februari, 2016. 

Katika kikao cha tarehe 02 februari, 2016 Bunge pamoja na mambo mengine lilijadili ripoti ya Kamati ya Bunge la Afrika Mashariki ya Masuala ya Mtangamano na Utatuzi wa Migogoro, ripoti hiyo iliyozungumzia Changamoto za kiusalama za utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Ukanda wa Kati wa Usafirishaji( Central Corridol). 

Akiwasilisha taarifa, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Abdullah Ally Hassan Mwinyi Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa upande wa Tanzania, alisema kamati hii ilitembelea Ukanda huu na kukutana na wadau mbalimbali na kwa kiasi kikubwa walitembelea Tanzania kwa kuwa kwa takribani 90% ya Ukanda huu iko upande wa Tanzania.

Wakiongea kwa wakati tofauti wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wameipongeza Tanzania kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa Umoja wa forodha na Soko la Pamoja, mafanikio haya ni kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Kamati ya Kitaifa ya Ufuatiliaji wa kuondoa Vikwazo visivyo vya Kiforodha (National Monitoring Committee on elimination of NTBs) na Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Soko la Pamoja (National Common Market Implementation Committee).

Kamati ya uondoaji Vikwazo visivyo vya kiforodha hadi Septemba,2015 imeweza kufanikisha kushughulikia jumla ya Vikwazo 87 kwa mara moja na ni vikwazo 18 tu ndio havijatatuliwa, kupunguza vizuizi vya barabarani katika Ukanda wa kati ( Road blocks) kutoka 56 hadi 6, Vizuizi hivyo vilivyobaki ni Vigwaza(Pwani), Mikese ( Morogoro), Nala(Dodoma), Njuki (Singida), Mwendakulima (Shinyanga) na Nyakahura (Kagera), kuweza kutoa jumla ya hati ya uasilia wa bidhaa( Certificates of Origin) 47,2333 kutoka July,2010 hadi June, 2015 na kuweza kuhamasisha wafanyabiashara wa ndani kutumia namba maalum za utambuzi wa bidhaa ( BARCODEs).

Kamati hii imepongeza ufanisi wa Mizani ya Vigwaza kwa kuwa na Teknologia ya Kisasa ambayo imeweza kupunguza muda wa kukagua mizigo na hivyo kuwapunguzia kero wasafirishaji, na Mizani za aina hizo zinatarajiwa kuwekwa katika kituo cha Manyoni (Singida) na Nyakanazi (Kagera) ili kuweza kubaki na Vituo vya Ukaguzi vitatu tu kwa upande wa Ukanda wa Kati.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Daniel Kidega, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya hasa katika kuhakikisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo amesema ni kitovu cha Usafirishaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Spika huyo amesema wanaafrika Mashariki wanajivunia kwa kazi yake nzuri anayofanya na kwa kipindi kifupi ameweza kuwa Rais wa mfano katika Ukanda wa Afrika Mashariki. 

Wabunge katika hatua nyingine wamesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za Mtangamano. Utekelezaji wa hatua hizi zote za Mtangamano utakuwa na mafanikio iwapo wananchi wa Afrika Mashariki watashirikishwa katika kila hatua kama Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya unavyobainisha katika kifungu cha 7.

No comments:

Post a Comment